Idadi ya waliofariki Misri yaongezeka

Watu wawili wameripotiwa kufariki katika makabiliano nje ya kanisa la Kikopti nchini Misri.

Duiru zinasema kuwa hali ya utulivu ilirejea katika eneo la Abbassiya ambako polisi walikuwa kwa wingi kudhibiti hali ya usalam. Eneo hilo linapakana na kanisa ambako makabiliano yalitokea.

Waandamanaji kadhaa wa ambao ni waumini wa kanisa hilo, walikusanyika katika eneo hilo mapema asubuhi ya leo

Makabiliano makali yalitokea nje ya kanisa hilo kufuatia mazishi ya wakristo wanne wa kikopti waliouawa katika ghasia za kidini siku ya Alhamisi.

Waombolezaji waliokuwa wanatoka katika kanisa hilo walikabiliana na wenyeji wa eneo hilo nje ya kanisa.

Polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kujaribi kuwatawanya waandamanaji. Zaidi ya watu 80 walijeruhiwa kwa mujibu wa shirika la kitaifa la habari.

Wizara ya afya ilisema kuwa mtu mmoja aliuawa katika ghasia hizo.

Waombolezaji awali walikuwa wakiimba nyimbo za kupinga serikali ya rais Mohammed Morsi.

Walioshuhudia vurugu hizo waliambia wanahabri kuwa ghasia zilianza baada ya umati wa watu kuvamia kikundi cha waombolezaji walipokuwa wanaondoka kanisani kwa kuwarushia mawe na mabomu ya petroli. Wakati huo pilisi walikuwa wachache sana katika eneo hilo.

Wakristo nao walijibu mashambulizi dhidi yao kwa kuwarushia mawe watu hao hadi polisi walipowasili katika eneo hilo na kujaribu kusitisha vurugu kwa kuwarushia watu gesi ya kutoa machozi

Duru zilisema kuwa barabara zilizoko karibu na eneo hilo zilikuwa na ghasia kati ya wakristo na watu wasiojulikana

Aidha moto uilianzishwa katika jengo lililokuwa karibu na kanisa hilo lakini moto huo ukazimwa kwa wakati.

Pia inaarifiwa kuwa Rais Morsi alilaani ghasia hizo kupitia kwa njia ya simu kwa papa Tawadros wa pili ambaye ndiye kiongozi kwa kanisa la kikopti.

''Shambulizi lolote dhidi ya kanisa hilo ni kama shambulizi dhidi yangu,'' alisema Papa Towadros ambaye pia aliwataka watu kuwa watulivu.