Wahisani waahidi dola bilioni 3.6 kwa Darfur

Image caption Hali ya njaa katika Darfur

Nchi wafadhili wa Darfur, wameahidi kutoa dola bilioni 3.6,za maendeleo na ukarabati wa jimbo la Darfur, kuweza kutolewa kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita ijayo.

Tangazo hilo limetolewa wakati wa kilele cha kongamano la kimataifa la siku mbili kuhusu Darfur nchini Qatar ilikuwa mwenyeji.

Waandalizi walitaka kuchangisha dola bilioni 7.2 za mpango wa maendeleo ambayo inalenga kuliweka jimbo hilo katika hali ya kujitegemea.

Takriban watu 300,000, wanaaminika kufariki wakati wa vita vya mwongo mmoja, katika jimbo la Darfur, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Wengine milioni 1.4 wanasalia kuwa wakimbizi.

Wakosoaji wanasema kuwa juhudi za kuleta amani katika jimbo hilo, zimehujumiwa kwani migogoro na migawanyiko haiishi katika jimbo hilo.

Maandamano yanayopinga kongamano hilo yalifanyika Darfur siku ya Ijumaa .

Wanaharakati wanasema kuwa maandamano yaliitishwa kwa sababu ukosefu wa usalama ulihujumu shughuli za ukarabati.

Pia wanasema kuwa wanapinga mkataba wa amani ulioafikiwa mwaka 2011 ambao ulitiwa saini nchini Qatar lakini ukakataliwa na makundi ya wapiganaji.

Hata hivyo, rasimu ya mkakati wa maendeleo, uliochapishwa kabla ya kuanza kwa mkutano, ulisema kuwa kucheleweshwa kwa shughuli hiyo utatatiza ukarabati.

Mgogoro katika jimbo la Darfur ulianza mwaka 2003 wakati waasi walipoanza kushambulia maslahi ya serikali na kutuhumu serikali ya Rais Bashir kwa kuwakandamiza waarabu weusi.

Kundi la wapiganaji wa kiarabu la Janjaweed lilituhumiwa kwa kuwaua waarabu weusi katika jimbo la Darfur

Ingawa ghasia katika jimbo hilo zimepungua, bado kuna makabiliano kati ya serikali na wanajeshi wa serikali, wapiganaji, wezi wa mifugo na makundi hasimu ya kikabila.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, anatakikana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kwa mauaji ya kimbare katika jimbo hilo.