Museveni ''ICC ilitumia vitisho kwa wakenya''

Image caption Rais wa Uganda, Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameituhumu mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kile alichotaja kutumia vitisho kama njia ya kuingilia uchaguzi wa Kenya.

Museveni aliyasema hayo wakati akiwahutubia wakenya na wageni waalikwa katika sherehe ya kuapishwa kwa Uhuru Kenyatta mjini Nairobi. Miongoni mwa wageni waalikwa walikuwa marais kadhaa wa Afrika na wanadiplomasia.

Uchaguzi huo ulifanyika mwezi Machi ambapo rais Kenyatta aliweza kumshinda mpinzani wake mkuu Raila Odinga.

Kenyatta na naibu wake Willima Ruto wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu katika mahakama ya ICC kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika miaka mitano iliyopita.

Kenyatta na Ruto wanatakiwa na mahakama hiyo kwani wamesmekana kuwa washukiwa wakuu wa ghasia hizo.

''Nataka kuwapongeza wapiga kura wa Kenya kwa swala lengine moja . Hatua ya kukataa vitisho vya mahakama ya ICC,'' alisema Museveni