Wanajeshi wa India wauawa Sudan Kusini

Haki miliki ya picha unmiss
Image caption Kikosi cha kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS

Wanajeshi watano wa kulinda amani kutoka India, waliokuwa wakisindikiza msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa, nchini Sudan Kusini, wameuawa na waasi.

Hii ni kwa mujibu wa duru kutoka kwa ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Walinda amani hao walikuwa wanafanya kazi katika kikosi cha wanajeshi wa umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini Unmiss. Walivamiwa na wapiganaji katika eneo la Jonglei

Maafisa wawili wakuu na wafanyakazi wa ujumbe wa UNMISS waliuawa katika shambulizi hilo. Watu wengine tisa walijeruhiwa.

Vurugu hizo zilitokea katika jimbo la Jonglei , maficho ya makundi ya wapiganaji.

Kikosi cha Unmiss kimekuwa Sudan Kusini tangu nchi hiyo kujitenga 2011, wakiwa na nia ya kulinda amani na usalama.

Katika taarifa yake, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema kuwa alishtushwa sana na shambulizi hilo na kuitaka serikali ya Sudan Kusini kuwachukulia hatua waliohusika.

Wizara ya mambo ya nje ya India ilisema kuwa inafanya mipango kupeleka miili ya wanajeshi hao nchini India kwa mazishi.

Wadadisi wanasema kuwa jimbo la Jonglei, limekumbwa na ghasia za kikabila tangu Sudan kusuini kujipatia uhuru mwaka 2011, Kaunty ya Pibor ikiathirika zaidi na pia ni sehemu ambapo walinda amani wa Umoja huo wanashika doria.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Kanali Philip Aguer, alilaumu wapiganaji wanaoongozwa na David Yau Yau kwa kufanya mashambulizi hayo. Sudan Kusini inadai kuwa muasi huyo anafadhiliwa na serikali ya Sudan.

Mkuu wa kikosi cha Unmiss Hilde Johnson, alisema kuwa serikali inatarajiwa kuanza harakati dhidi ya wapiganji hao watiifu kwa bwana Yau Yau katika eneo la Jonglei.

Hali ya utovu wa usalama, imekithiri kutokana na mzozo wa wizi wa mifugo kati ya makundi ya kikabila na kuwaacha watu wengi wakiwa wamefariki na maefu ya wengine kuachwa bila makao.

India inachangia pakubwa katika kikosi cha walinda amani wa umoja wa Mataifa kote duniani na imekumbwa sana na tatizo la walinda amani wao kuuwa katika siku za nyuma.