Malawi 'Maddona ajifunze kusema ukweli'

Malawi, imemtuhumu muimbaji wa Marekani Madonna kwa kuwadhulumu maafisa wa serikali baada ya kulalamika kuhusu alivyopokelewa alipoizuru nchi hiyo.

Madonna ambaye ameasili watoto wawili kutoka Malawi , alizuru shule kumi ambazo anazifadhili nchini humo hivi karibuni.

Serikali ilimtuhumu kwa kuongeza chumvi msaada wake nchini humo na kutaka kushughulikiwa kama mtu muhimu sana.

Msimamizi mkuu wa Madonna, Trevor Neilson, alituhumu serikali kwa kuwa na kisasi na shirika la misaada la mwimbaji huyo, Raising Malawi.

Katika taarifa yake kwa BBC , Neilson pia aliwatuhumu maafisa wa serikali kwa kutumia vibaya pesa za zinazonuiwa kusaidia shule na hata kunyanyasa mashirika ambayo Madonna alikuwa ametoa msaada kwao.

Inasemekana Madonna aliudhiwa kuwa yeye na kikosi chake walivuliwa hadhi ya wageni waheshimiwa walipokuwa wanaondoka nchini humo.

Iliwabidi kupanga foleni na abiria wengine katika uwanja wa ndege na kukaguliwa na maafisa wa usalama.

Serikali ilitoa taarifa kali kuzungumzia tukio hilo na kusema kuwa Madonna anahitaji kujifunza kuwa ni muhimu kusema ukweli na kusema kuwa sio lazima kwa Madonna kupokea au kupewa hadi ya wageni waheshimiwa kwani serikali ndio inaamua.

Walimtuhumu kwa kusema kuwa ni muimbaji wa kimataifa ambaye anadhani kuwa lazima atambulike kwa kuwanyanyasa maafisa wakuu wa serikali badala ya kucheza muziki wa heshima akiwa kwenye jukwaa.

Ilisisitiza kuwa Madonna lazima ajifunze kusema ukweli, kwani kuambia dunia nzima kuwa anajenga shule nchini Malawi wakati anachangia tu kujenga madarasa haiendi sambamba na mtu ambaye anataka kupewa hadhi ya wageni waheshimiwa.