John Kerry azuru Uchina

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, anafanya mazungumzo na viongozi wa Uchina mjini Beijing, baada ya kuwasihi wachukue msimamo mkali kuhusu Korea Kaskazini kwa sababu ya mpango wake wa kuunda silaha za nuklia.

Kwanza alikutana na Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje, Wang Yi, ambaye alisema ziara hiyo ya Bwana Kerry inatokea wakati muhimu.

Bwana Kerry alisema Uchina ina kauli kubwa zaidi juu ya Korea Kaskazini kushinda mtu yeyote yule, na aliisihi ifanye juhudi zaidi kumzuwia jirani na mshirika wake.

Korea Kaskazini inaitegemea Uchina kwa biashara na msaada mwingi pamoja na msaada wa kidiplomasia.

Ijumaa Bwana Kerry alionya kwamba kombora ambalo Korea Kaskazini inatarajiwa kurusha litazidisha hali ya hatari ilioko.