Al-Shabaab wafanya mashambulio Mogadishu

Watu waliokuwa na silaha wamefanya mashambulio mawili mjini Mogadishu, Somalia, na kuwauwa watu kama 20.

Katika shambulio la kwanza risasi nyingi zilifyatuliwa pamoja na miripuko kadha ndani ya jengo la mahakama makuu ambalo lilikuwa limejaa watu waliojaribu kukimbia.

Waziri mmoja wa serikali alieleza kuwa washambuliaji tisa walihusika na wote sasa wameuwawa.

Sita walikufa walipojiripua.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab linasema walifanya shambulio hilo, na kwamba wapiganaji wao sita walikufa.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, Mahamed Ali, alisema aliwaona baadhi ya watu waliokufa ndani ya mahakama:

"Nimeona maiti nyingi ndani ya mahakama na mimi nimebahatika sana kunusurika.

Ni shida kueleza."