Wanajeshi wa Chad waanza kuondoka Mali

Image caption Wanajeshi wa Chad

Serikali ya Chad, moja ya nchi iliyochangia idadi kubwa ya wanajeshi kushika doria nchini Mali, imeanza kuwaondoa wanajeshi wake kutoka nchini humo. Taarifa hii ni kwa mujibu wa rais wa nchi hiyo Idriss Deby.

''Jeshi la Chad halina uzoefu wa kupigana katika mazingira ya mashambulizi ya kuvizia ambayo ndio yanafanyika nchini Mali,'' alisema rais Derby.

Wanajeshi watatu wa Chad, waliuawa katika shambulizi la kujitoa mhanga siku ya Ijumaa.

Aidha wanajeshi kutoka Chad , Ufaransa na nchi zengine za kiafrika, wamefurushawapiganaji wa kiisilamu kutoka miji iliyo Kaskazini mwa Mali.

Lakini makabiliano yangali yanaendelea katika sehemu zengine za jangwa la Sahara.

Wanajeshi 2,000 wa Chad walikuwa na jukumu kubwa sana katika vita hivi hasa kwa sababu ya uzoefu wao kupigana vita vya jangwani.

Takriban wanajeshi 30 wameuawa ikiwa idadi kubwa kulinganishwa na wanajeshi kutoka nchi nyingine yoyote.

Watatu kati yao waliuawa katika shambulizi la kujitoa mhanga mjini Kidal siku ya Ijumaa.

Rais Deby aliambia vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa wanajeshi wake wameshatekeleza wajibu wao.

Ufaransa pia imeanza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake 4,000 ikitaka kusalia na wanajeshi 1,000 nchini humo mwishoni mwa mwaka.

Ufaransa iliongoza kampeni ya kuwapeleka wanajeshi nchini Mali mwezi Januari, ikisema kuwa wapiganaji wa al-Qaeda, walitishia kuvamia mji mkuu, Bamako.