Uchumi wa Afrika wakuwa kwa kasi

Ukuwaji wa uchumi Kusini mwa jangwa la Sahara, unakisiwa utakuwa pakubwa ikilinganishwa na sehemu zengine duniani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa utabiri wa benki ya dunia.

Upatikanaji wa bidhaa, uwekezaji mkubwa pamoja na uchumi wa dunia kuanza kuimarika haya yote yanapaswa kupiga jeki uchumi wa bara la Afrika kwa asilimia tano.

Lakini benki ya dunia inasema kuwa serikali za Afrika zina jukumu kubwa kuhakikisha kuwa uchumi unakuwa kwa kiwango hicho pamoja na kupunguza umaskini.

Mwaka huu uchumi wa dunia unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 2.4.

Ripoti hiyo imesema kuwa ukuwaji mkubwa wa uchumi barani Afrika ulikuwa umepunguza viwango vya umaskini katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Takwimu za benki hiyo zilionyesha kuwa idadi ya waafrika wanaopata chini ya dola moja ilishuka kutoka asilimia 58 hadi asilimia 48.5 kati ya mwaka 1996 na 2010.

Benki hiyo imesema kuwa changamoto kubwa kwa ukuwaji wa uchumi ni kuongezeka kwa pengo kati ya maskini na matajiri na pia kutegemea sana mapato yanayotokana na madini kwa nchi kadhaa za Afrika.

Nchi zenye utajiri mkubwa wa madini kama vile Equatorial Guinea, Nigeria na Gabon zimeonekana kama nchi zisizofanya jitihada kukabiliana na umaskini ikilinagnishwa na nchi zingine Afrika zilizo na maliasili ndogo.

Benki hiyo imetilia mkazo maendeleo na ujenzi wa miundo mbinu kuhakikisha ukuwaji mkubwa wa uchumi.