8 wauawa mjini Garissa, Kenya

Watu wanane wameuawa katika shambulizi lililofanywa na watu waliokuwa wamejihami mjini Garissa Mashariki mwa Kenya.

Walioshuhudia shambulio hilo walisema kuwa washambuliaji walilenga kushambulia hoteli moja kabla ya kutoweka.

Watu watano walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini na shirika la Red Cross.

Kenya imekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara tangu wanajeshi wake kwenda Somalia kupambana na wapiganaji wa kundi la al-Shabab mwaka 2011.

Polisi walithibitisha kuwa wangali wanaendesha harakati zao kuwasaka washukiwa.

Mji wa Garissa umekumbwa na mashambulizi kadhaa katika miezi ya hivi karibuni. Mnamo mwezi Januari, mashambulizi mengine yalifanyika mjini humo ambapo watu watano waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa.

Mwezi Oktoba watu waliokuwa wamejihami pia walimuua polisi mmoja kwa kumpiga risasi huku wakimjeruhi mwingine. Pia mwezi wa Novemba wanajeshi watatu na polisi wawili wa Kenya waliuawa mjini humo.

Mashambulizi haya yanasemekana kufanywa na al-Shabab kama ya kulipiza kisasi dhidi ya harakati za jeshi la Kenya nchini Somalia.

Mwezi Novemba, ghasia zilitokea mjini Nairobi, baada ya vijana walioghadhabishwa kulaumu wasomali kwa mashambulizi ya bomu yaliyokea.