Priscah wa Kenya ashinda London marathon

Wakimbiaji wa kwanza katika mbio za London wameshamaliza na Priscah Jeptoo wa Kenya ameshinda mbio za wanawake na raia wa Ethiopia, Tsegaye Kebede, ametokea wa kwanza upande wa wanaume.

Marathon hiyo imefanywa siku sita baada ya mashambulio katika marathon ya mjini Boston, Marekani.

Ulinzi ulikuwa mkubwa lakini hakuna ripoti za kutokea lolote.

Watu waliokufa Boston walikumbukwa mjini London kwa watu kukaa kimya kwa sekunde 30 kabla ya mashindano kuanza, na wakimbiaji waliombwa wavae kitambaa cheusi.

Watu zaidi ya 30,000 walishiriki kwenye mashindano hayo na malaki walishangilia kando ya mabarabara.