Mchango wa Museveni wazua mjadala

Image caption Rais Yoweri Museveni

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekabidhi kikundi cha vijana mfuko uliokuwa na dola laki moja pesa taslimu na hivyo kuzua maswali kuhusu lengo la matumizi ya pesa hizo.

Mchango huo uliotolewa ulionyeshwa wazi kwa televisheni, huku watu wakilaani hatua hiyo kwa mitandao ya kijamii.

''Kungekuwa na mfumo wa kuhakikisha kuwa vijana wanatumia vyema pesa hizo,'' alisema mdadisi mmoja kwa jina Peter Magelah.

Naye waziri mmoja alinukuliwa akisema kuwa kutoa pesa hizo kwa njia ya wazi hadharani kunaonyesha uwazi.

Museveni aliahidi kusaidia vijana wakati wa kampeini zake mnamo mwaka 2011.

Waziri anayehusika na maswala ya Rais Frank Tumwebaze, alisema kuwa Rais anaunga mkono miradi ya vijana ya kujikimu kimaisha.

Wengi walishangilia wakati Rais Museveni alipotoa mfuko huo wenye shilingi milioni 250 pesa za Uganda kabla ya kuwakabidhi waakilishi wa vijana katika eneo la Busoga.

Wakati huohuo, aliwakabidhi vijana hao basi dogo , lori na pikipiki 15.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala anasema kuwa vijana wamezoea kumuona Rais akitoa pesa hadharani hasa katika hafla za hadhara.

Lakini kilichowashangaza wananchi wengi ni kiasi cha pesa zilizotolewa na picha inayomuonyesha Museveni akishikilia mfuko wenye pesa.

Waganda wengi wanaotumia mtandao wa kijamii wa Twitter, wamekuwa wakitoa maoni yao, kuhusu kitendo cha Rais.

Bwana Peter Magelah, amesema kuwa hizi tu ni mbinu za kisiasa za Rais Museveni kujipatia umaarufu.

"je tunafahamu vipi pesa hizo zitatumiwa, hakuna njia ya kuhakikisha zimetumiwa ipasavyo.Hakuna njia ya kuhakikisha kuwa kuwa pesa hizo zitarejeshwa ikiwa zitatumiwa vibaya. Ni hasara kubwa kwa nchi.''