Bouteflika auguzwa ng'ambo

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, amesafirishwa na kupelekwa hospitali ya Paris baada ya kupata ugonjwa wa kiarusi kidogo.

Wakuu wa Algeria wanasema Bwana Bouteflika alipelekwa Paris kufuata pendekezo la daktari wake lakini hali yake si ya kutia wasiwasi.

Rais Bouteflika, mwenye umri wa miaka 76, anaonekana hadharani mara chache tu, na amekuwa akiuguwa kwa miaka kadha.

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa Jumamosi alipata ugonjwa wa kiarusi kidogo lakini haifikiriwa afya yake itaathirika kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu wa Algeria alisema hali ya rais siyo mbaya.

Lakini kwa vile amesafirishwa na kupelekwa Paris, Ufaransa, watu wanauliza kama taarifa rasmi inaeleza ukweli.

Bwana Bouteflika alifanyiwa upasuaji kwenye hospitali mjini Paris miaka kadha iliyopita.

Taarifa rasmi ilieleza kwamba alikuwa na kidonda cha tumbo; lakini nyaraka za siri za wana-diplomasi wa Marekani zilipofichuka zilisema kumbe alikuwa na saratani.

Kuna watu wanaoamini kuwa Bwana Bouteflika anaweza kugombea muhula wane katika uchaguzi wa mwaka ujao, juu ya umri na afya yake.

Yeye ni mmoja kati ya viongozi wakongwe ambao wameshikilia madaraka katika siasa za Algeria tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa zaidi ya miaka 50 iliyopita.