Mgogoro kuhusu mahakama Misri kutatuliwa

Image caption Rais Mohammed Morsi

Duru kutoka kwa ofisi ya rais wa Misri Mohammed Morsi zinasema kuwa huenda mwafaka umeafikiwa ili kumaliza mzozo uliopo kuhusu idara ya mahakama.

Baada ya mzungumzo na maafisa wakuu wa idara ya mahakama, Jumapili, rais Morsi alisema kuwa kongamano litaandaliwa wiki hii kutoa nafasi ya kuwalisha malalamiko yoyote na kuwa atakubali uamuzi utakaotolewa.

Mpango wa kupunguza umri wa majaji kuweza kustaafu ulikuwa umetishia nyadhifa za maelfu ya majaji na hivyo kuighadhabisha idara ya mahakama.

Bwana Morsi amekuwa katika mzozano na idara ya mahakama tangu aingie mamlakani mwezi Juni mwaka jana.

Washirika wake katika chama cha Muslim Brotherhood, wanasema kuwa mahakama imejaa majaji waliokuwa wanamuunga mkono rais wa zamani Hosni Mubarak.

Nao wapinzani wa Morsi wanasema kuwa anajaribu kujaza nafasi hizo na wafuasi wake.

Mgogoro ulikithiri wiki jana wakati bunge lilipoendelea kujadili mswaada unaonuia kupunguza umri ambao majaji wanaweza kustaafu kutoka miaka 70 hadi 60, hali itakayowaathiri majaji 13,000 na viongozi wa mashtaka.

Mswaada huo pia ungezuia mageuzi katika idara ya mahakama kuhusu mamlaka ya Rais aliyojiongezea mwaka jana.

Maandamano dhidi ya mswaada huo yalipangwa kufanyika Jumatatu ingawa kwa sasa yamefutiliwa mbali.