Ni lini mapigano yataisha Darfur?

Muongo mmoja baada ya vita mbaya ya Darfur kuanza hakuna dalili ya kumalizika kwa mapigano.

Kasi ya mapigano katika mkoa huo wa magharibi mwa Sudan imepungua tangu miaka ya awali, lakini sehemu kubwa ya Darfur bado ni hatari sana.

Zaidi ya watu milioni 1.4 ya watu wanaishi kwa kutegemea msaada wa chakula katika kambi zilizotapakaa Darfur, na wengine wengi wameikimbia nchi.

Mgogoro huo wenye utata mwingi pia umesababisha kuvurugika kwa taswira ya Sudan duniani. Marekani na wanaharakati wengi wa nchi za magharibi wameishutumu serikali ya Sudan kwa kutekeleza mauaji ya kimbari.

Hata kabla vita havijalipuka, tayari Darfur ilikuwa kwenye matatizo. Kama ilivyo kwa mikoa mingine ya himaya ya Sudan, haikuwahi kuendelezwa na ilitengwa kisiasa.

Kupungua kwa mvua kwa miongo mingi kumesababisha maisha kutetereka huko Darfur na kupelekea upungufu wa mara kwa mara wa chakula.

Lakini, jambo la kushangaza, licha ya hali hiyo, kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya vikundi vya kikabila vikigombea haki ya kumiliki ardhi au kwa jina la huko inafahamika kama “Hakurat”.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, kundi la vuguvugu la Kiarabu liliibuka likisemekana kuungwa mkono na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Asili ya watu wa Darfur ni suala tete na gumu, lakini makundi ya Waafrika kama ya Fur, Zaghawa na Masalit yanahisi kwamba, serikali inawapendelea Waarabu. Dini haikuwa suala nyeti, kila mtu Darfur ni Mwislamu.

Inaelezwa kuwa, mwanzo wa vita ya Darfur ulikuwa 2003, ingawa vikundi vya waasi vilianzishwa kabla ya mwaka huo.

Mnamo 2008, Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba, watu 300,000 waliuawa kutokana na vita hivyo, ingawa Khartoum inapinga idadi hiyo.

Rais wa Sudan, Omar Hassan Al Bashir, ameshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwa makosa ya mauaji ya kimbari,uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu makosa yaliyotekelezwa Darfur.

Rais Bashir anakuwa kiongozi wa kwanza aliyeko madarakani kutolewa kwa hati ya kumkamata na ICC. Yeye pamoja na maafisa wengine waandamizi wanaokabiliwa na mashtaka kama hayo, wote wameyakanusha.

Image caption Kiongozi wa waasi wa Darfur aliyeuawa mapema mwezi aPRILI

Nchi za magharibi hazitaki chochote kutoka kwa Rais Bashir ama serikali yake. Wanadiplomasia hawatakutana naye, na kuna uwezekano mdogo wa Sudan kusamehewa deni lake kubwa ama vikwazo vya Marekani kuondolewa iwapo ataendelea kuwepo madarakani.

Rais Bashir anashawishika kwamba, Marekani inajaribu kumuondoa madarakani, wakati Sudan ikitegemea uungwaji mkono katika Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kutoka kwa China na Russia.

Lakini matatizo ya Darfur hayatamalizika hadi hapo suluhisho lipatikane kwa matatizo ya kudumaa kwa maendeleo, kutengwa kisiasa na kudidimia kwa rasilimali