Watoto walevamu Ghana wapata afueni

Viongozi wa kijadi kaskazini mwa Ghana wamekubaliana kumaliza vitendo vya mauaji ya watoto wachanga wenye ulemavu ambao inaaminika walikuwa na pepo.

Watoto wenye ulemavu walionekana kama wenye mkosi hivyo walinyweshwa sumu ili kuwaua.

Mmoja wa wanaharakati ameiambia BBC kwamba, kuboreshwa kwa huduma za afya na elimu kumesababisha kupungua kwa imani hizo potofu.

Mwanaharakati Raymond Ayine, amepongeza uamuzi huo ambao utahusisha miji saba. Lakini akadai kwamba, hakuna uhakika kama mauaji hayo yamezuiwa nchi nzima.

Mwandishi wa BBC, Vera Kwakofi, anasema mkoa wa Kasena Nankana ambako uamuzi huo umetangazwa ni eneo ambalo imani hiyo ilikuwa imeshamiri.

Wakati mwingine watoto waliozaliwa na kuhisiwa kuwa ni mkosi katika familia pia walituhumiwa kuwa watoto wenye mapepo nao waliuawa.

Kundi la wanaume waliokuwa wakiwapa sumu watoto, sasa wamepewa majukumu mapya ambapo watafanya kazi na watoto hao walemavu kuhamasisha haki zao.

Mwandishi mmoja wa habari za kiuchunguzi, Anas Aremeyaw, ameiambia BBC kwamba, alichukua mwanasesere na kumpeleka kwa mtabiri, na kumwambia kuwa huyo alikuwa mtoto mwenye matatizo ya kula chakula na ulemavu wa viungo.

Baada ya mtabiri huyo kuzungumza na mizimu huku akiruka juu na chini, na baada ya hapo alidai kwamba, mizimu imethibitisha kwamba, mtoto huyo ana mapepo na anastahili kuuawa mara moja na pia mtoto huyo tayari amekwishawaua watu wawili wa familia yake.

Mmoja wa viongozi wa kijadi, Naba Henry Abawine Amenga Etigo, amesema kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote atakayekamatwa akijaribu kuwadhuru tena watoto wenye ulemavu atakabidhiwa kwa polisi.

Bwana Ayine, kutoka kundi la wanaharakati la Afrikids, amesema amesikitishwa kwamba, katika zama hizi, mtoto anaweza kupoteza maisha yake kwa sababu ya vitendo hivi vya kikatili.

Amebainisha kuwa, katika maeneo ya vijijini ambako imani hizo zimeenea, wanawake kwa kawaida hujifungua bila kupata huduma za wauguzi na hata vipimo kabla ya kujifungua. Kutokana na hali hiyo, akina mama wajawazito hupata matatizo wakati wa kujifungua kuliko sehemu nyingine.

Amefafanua kuwa, hata kabla ya mauaji hayo kupigwa marufuku rasmi, hakukuwa na takwimu zilizohifadhiwa kuhusu mauaji ya watoto wenye pepo katika eneo hilo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Ghana, wanawake vikongwe wanaotuhumiwa kwa uchawi, wakati mwingine hulazimika kuhama makazi yao na kwenda kuishi kwenye kambi rasmi za watu wanaotuhumiwa kwa uchawi.