Mwanajeshi wa Ufaransa auawa Mali

Image caption Ufaransa inatarajiwa kuanza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Mali

Mwanajeshi mmoja wa Ufaransa nchini Mali ameuawa na wengine wawili kujeruhiwa vibaya.

Kwa mujibu wa maafisa wa Ufaransa, mwanajeshi huyo kutoka kikosi maalum cha Ufaransa aliuawa Magharibi mwa nchi baada ya gari lake kulipukiwa na bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara.

Hadi kufikia sasa wanajeshi sita wa Ufaransa wameuawa tangu Ufaransa kuanza operesheni yake dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu waliokuwa wanadhibiti Kaskazini mwa nchi

Ufaransa ilitangaza kuanza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake 4,000 walioko Mali.

Lakini wengine 1,000 watasalia nchini humo hadi mwakani kuweza kukabiliana na wapiganaji wa kiisilamu walio na uhusiano na kundi la Al-Qaeda

Baadhi ya miji, imeweza kudhibitiwa na wanajeshi hao, lakini wapiganaji hao wangali kwenye maficho yao ya mwisho Kaskazini mwa Mali ambako wanafanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya wanajeshi wa Mali na Ufaransa.

Hivi maajuzi Umoja wa Mataifa uliafikia kunda kikosi cha wanajeshi 12,000 kushika doria nchini Mali.

Watashirikiana na kikosi cha wanajeshi 6000 ambao tayari wako nchini humo.

Rais Francois Hollande ametoa rambi rambi zake kwa familia za waliouawa huku akiwasifu kwa ujasiri wao nchini Mali.