ANC chajitetea kuhusu picha yao na Mandela

Image caption Nelson Mandela alilazwa hospitalini kwa siku kumi alipokuwa anatibiwa homa ya mapafu

Chama tawala nchini Afrika Kusini, cha African National Congress, ANC, kimetetea kitendo chake cha kumpiga picha kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela wakati viongozi wa chama hicho walipomtembelea.

Kimesema kitendo hicho si cha kujitafutia umaarufu.

Hizo zilikuwa picha za kwanza za rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini tangu alipotoka hospitali mnamo Aprili 6 mwaka huu baada ya kulazwa kwa takriban wiki moja akisumbuliwa na ugonjwa wa Homa ya Mapafu.

Bwana Mandela alionekana kushangaa huku akiwa amezungukwa na viongozi wa ANC na watu waliokwenda kumjulia hali. Msemaji wa ANC, amesema chama hicho kimefurahi kuionesha dunia picha za kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 94, hata katika hali yake tete.

Picha za video nadra za Bwana Mandela ambaye anafahamika kwa jina lake la ukoo kama "Madiba" , zilionyeshwa na kituo cha televisheni cha taifa cha Afrika Kusini, SABC.

Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg, Milton Nkosi anasema, kumekuwa na malalamiko kwenye mitandao ya kijamii hasa wa Twitter, ambako mjadala huo unaendelea kuhusu kuoneshwa kwa video hiyo.

Wengi wanaona hatua hiyo kama ukandamizaji na kuingilia maisha binafsi ya rais huyo wa zamani.

Katika picha hizo, Bwana Mandela anaonekana akiwa hatabasamu, amekaa wima kwenye kochi na miguu yake imefunikwa na blanketi huku watu wakimpiga picha kwa kutumia kamera zao.

"Mara kadhaa vyombo vya habari nchini humo vimekuwa vikionywa na ANC na serikali ya Afrika Kusini, kuhusu kuheshimu maisha binafsi ya Madiba, na sasa tunajua jinsi wanavyomchukulia", ameandika mtu mmoja kwenye mtandao wa Twitter.

Rais Jacob Zuma na Naibu Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa walikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa ANC waliomtembelea Bwana Mandela nyumbani kwake jijini Johannesburg siku ya Jumatatu na walipewa maelezo kuhusu maendeleo ya afya yake na jopo la madaktari.

Image caption Rais Jacob Zuma alipomtembelea Mzee Nelson Mandela

Rais Zuma amesema, Bwana Mandela aliwashika mikono watu na hata kutabasamu.

Msemaji wa ANC, Jackson Mthembu, amekaririwa akisema kuwa, "Wale wanaolalamika kwamba, picha za hivi karibuni za Madiba ni njia ya kujipatia umaarufu kwa chama cha ANC, wanakula zabibu chungu".

Akaongeza kuwa, watu wetu hawajamuona Madiba miaka mingi. Na sasa wamemuona akifungua na kufunga macho yake, tunafurahia afya yake. Na sasa sio kijana mdogo tena.

Afya ya Bwana Mandela imekua ikiendelea kuzua wasiwasi katika siku za hivi karibuni. Matatizo ya mapafu ya kiongozi huyo mkongwe yalianza miaka 27 iliyopita tangu alipokuwa mfungwa wa kisiasa.

Alikaa gerezani kwenye upepo mkali katika kisiwa cha Robben kwa miaka 18 ambako alipatwa na amradhi ya Kifua Kikuu.

Disemba mwaka jana alilazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili akipatiwa matibabu ya mapafu na mawe kwenye mfuko wa nyongo. Na Februari mwaka huu madaktari walimpatia tiba ya matatizo ya tumbo.

Bwana Mandela ambaye aliondoka madarakani kama rais mwaka 1999, anaheshimika nchini Afrika Kusini kutokana na mchango wake wa kumaliza mfumo wa ubaguzi ama utawala wa wazungu wachache.

Alistaafu kushiriki shughuli za kijamii mwaka 2004, baada ya kuwa kama balozi mwenye hadhi ya juu wa nchi hiyo .

Bwana Mandela alikuwa rais wa kwanza Mwafrika katika miaka ya tisini na anaonekana na wengi kama baba wa taifa hilo Alitunukiwa nishani ya Amani ya Nobel mwaka 1993 pamoja na rais wa zamani FW de Klerk, kwa kumaliza ubaguzi wa rangi na kuleta demokrasia nchini Afrika Kusini.