Athari za vita vya Iraq kwa watoto

Image caption Watoto wengi wamethirika na vita nchini Iraq

Miaka kumi tangu George W Bush kutangaza kukamilika kwa vita nchini Iraq, shirika la misaada lijulikanalo kama War Child limeelezea hali nchini humo kuwa mojawapo ya mizozo iliyopuuzwa duniani.

Linasema kwamba takribani watoto 700 na vijana walio na umri chini ya miaka 25 wamefariki katika ghasia nchini humo katika muda wa miezi mitano iliyopita pekee.

Na watoto walio na umri wa miaka 14 wamesajiliwa na kutumiwa kama walipuaji wa kujitoa muhanga.

Shirika la War Child linasema Iraq ni mojawapo ya maeneo mabaya zaidi katika eneo zima la mashariki ya kati kuwepo mtoto.Na sio ghasia tu zinazowaua, na kuwadhalilisha watoto.

Ni athari za moja kwa moja kwa watoto hao.

Licha ya kwamba Iraq sasa ni nchi ya kipato cha kiwango cha wastani ikiwa na utajiri mkubwa wa mafuta, mtoto mmoja kati ya wanne wanaathirika na utapia mlo kutokana na lishe duni.

War Child inasema watoto Iraq wako nyuma katika masomo huku idadi ndogo ya wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wakiwa katika shule za upili.

Ujumbe wa shirika hilo ni kwamba operesheni nchini humo haikukamilika kama alivyosema rais Bush.War Child linasema msada wa kila mwaka umepungua kutoka dola bilioni 20 mnamo mwaka 2005 hadi bilioni moja na nusu mwaka 2011.

Huku ghasia zikizidi shirika hilo limetoa wito kwa wafadhili kutoa usaidizi wa muda mrefu kwa Iraq unaolenga mahitaji ya watoto.

Lakini kuna shutuma inayofichika pia kuhusu umuhimu wa mambo ndani ya Iraq kwenyewe.

Pendekezo moja katika ripoti ya shirika hilo ni kuwa wafadhili wa kiamataifa wanapaswa kushinikiza mashirika ya kijamii nchini humo ili serikali iweze kuwajibishwa kuhusu utoaji wake wa huduma.