Wanajeshi wadaiwa kuhusika na maafa Baga

Nyumba zilizoharibiwa Baga
Image caption Nyumba zilizoharibiwa Baga

Picha za satelite zimeonyesha kuwa nyumba 2,275 ziliharibiwa wakati wa operesheni ya kijeshi ya kuwasaka wapiganaji wa Kiislamu mjini Baga Kaskazini mwa Nigeria mwezi uliopita.

Haya ni kwa mujibu wa shirika moja la kutetea haki za kibinadam la Human Rights Watch.

Shirika hilo limedai kuwa wanajeshi hao walifanya uharibifu mkubwa badala la kulinda raia na mali yao baada ya wapiganaji wa Boko Haram kushambulia kituo kimoja cha kijeshi.

Jeshi la Nigeria halijasema lolote kuhusu madai hayo.

Kuna ripoti za kutatanisha kuhusu idadi ya watu waliouawa huku shirika hilo likidai kuwa watu 37, waliuawa, lakini mashirika mengine yamesema zaidi ya watu mia moja themanini waliuawa.

Wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram, limeendelea mashambulio makali katika eneo hilo, wakitaka kubuniswa kwa jimbo lenye utawala unaozingatia sheria za Kiislamu tangu mwaka wa 2010.

Wapiganaji wa Boko Haram

Image caption Gari la jeshi lililoshambuliwa na wapiganaji wa Boko Haram nchini Nigeria

Waandishi wa Habari wanasema wanajeshi wa serikali wameshutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa harakati zao za kuwasaka wapiganaji hao wa waasi.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, ameitaja mzozo huo katika eneo la Baga kuwa jambo la kusitisha na ambalo halikubaliki kamwe.

Shirika hilo la Human Rights Watch limetoa wito kwa utawala wa Nigeria kuchunguza na kuwafungulia mashtaka wanajeshi ambao wanatuhumiwa kuhusika na ghasia hizo za Baga.

Shirika hilo limenadi kuwa uchunguzi wa picha za satelite zimethibitisha kuwa habari zilizotolewa na jeshi kuwa nyumba thelathini ziliharibiwa wakati wa mapigano hayo ya Baga kati ya April kumi na saba na Kumi na nane mwaka huu ni ya uongo.

Wakaazi wa mji wa Baga waliliambia shirika hilo kuwa wanajeshi hao walifanya operesheni kali ya nyumba hadi nyumba baada ya wapiaganaji wa Boko Haram kumuua mwanajeshi ambayo ambaye alikuwa akishika doria katika kituo kimoja cha ukaguzi.