Waziri mkuu India akerwa na mauaji

Waziri Mkuu wa India,Manmohan Singh ametaka wale waliohusika na kifo katika gereza moja nchini Pakistan cha Sarabjit Singh raia wa India aliyekuwa akituhumiwa kwa ujasusi kuchukuliwa hatua za kisheria.

Sarabjit Singh alifariki dunia baada ya kupigwa kwa matofali na wafungwa wengine katika gereza la Kot Lakhpat lililopo Lahore siku ya Ijumaa iliyopita.

Alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama moja ya Pakistan mwaka 1991.

Katika taarifa yake, Manmohan Singh, amemuelezea Sarabjit Singh, kama mtoto shupavu wa India na kusema kuwa kitendo cha kumpiga ni cha kikatili.

"Kimsingi inasikitisha kwamba serikali ya Pakistan haikusikia kilio cha serikali ya India, familia ya Sarbjit na jamii ya India na Pakistan kuitazama kesi hii kwa jicho la kibinadamu," ameongeza Manmohan.

Sarabjit Singh alipoteza fahamu na kufariki dunia Alhamisi asubuhi katika hospitali ya Jinnah mjini Lahore. Alikuwa amehukumiwa kifo kufuatia tuhuma za ujasusi dhidi yake na pia ushiriki wake katika mashambulio ya mabomu yaliyoua watu 14 nchini Pakistan mwaka 1990.

Familia ya Sarabjit ambayo ilikuwa imerejea India baada ya kumtembelea hospitali nchini Pakistan, daima imekua ikisisitiza kwamba, alikuwa hana makosa na kuwa aliingia Pakistan kimakosa wakati anakamatwa.

Lakini wito wa kutaka asamehewe ulikataliwa na mahakama za Pakistan na pia rais wa zamani Pervez Musharraf.

India ilitoa wito kwa Sarabjit Singh, mwenye umri wa miaka 49, aachiliwe huru ama arejeshwe India kufuatia wasiwasi baada ya kushambuliwa. Alipata majeraha makubwa ikiwemo kuvunjika kwa fuvu la kichwa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, imesema kuwa, Sarabjit Singh alipatiwa huduma bora kabisa na kwamba, wauguzi katika hospitali ya Jinnah walikuwa wakimhudumia muda wote ili kuokoa maisha yake.

Maafisa wa India na Pakistan wanasema wanaandaa mipango ya kuurejesha mwili wa Sarabjit. Suala hilo linahofiwa huenda likaibua upya mvutano katika uhusiano wa mataifa hayo jirani yanayomiliki silaha za nuklia na mahasimu wa muda mrefu.

Mara kwa mara Pakistan na India zimekuwa zikiwakamata raia wa upande mwingine zikiwatuhumu kuwa majasusi mara baada ya kuvuka mpaka wa nchi kavu au maji. xtmuid.yahoo.com