Korea Kaskazini yamhukumu Mmarekani jela

Image caption Kenneth Bae (Kulia)

Korea Kaskazini imesema imemhukumu raia wa Marekani kifungo cha miaka 15 jela na kazi nzito.

Tangazo hilo limetolewa na Shirika la Habari la Taifa, KCNA, na limesema kuwa, Pae Jun – Ho, anayetambulika nchini Marekani kama Kenneth Bae, alihukumiwa Aprili 30 mwaka huu.

Alikamatwa mwaka jana baada ya kuingia Korea Kaskazini kama mtalii. Pyongyang inasema alituhumiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya serikali.

Hatua ya kufungwa kwa raia huyo imekuja wakati kukiwa na hali tete kati ya Marekani na Korea Kaskazini, baada ya Pyongyang kufanya jaribio la tatu la nuklia.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini wiki iliyopita vilisema kuwa, Bwana Pae alikiri makosa ya uhalifu dhidi ya Korea Kaskazini ikiwemo jaribio la kuipindua serikali.

Bwana Pae, mwenye umri wa miaka 44, alikamatwa Novemba mwaka jana wakati akiingia katika bandari ya kaskazini mashariki katika mji wa Rason, ambao ni ukanda maalum wa kiuchumi karibu na mpaka wa Korea Kaskazini na China.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Patrick Ventrell, ameitaka Korea Kaskazini kumuachia huru Kenneth Bae mara moja chini ya misingi ya kibinadamu.

Korea Kaskazini imewakamata raia kadhaa wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni, wakiwemo waandishi wa habari na waumini wa dini ya Kikristo ikiwatuhumu kwa kuwabadili wananchi wake imani zao za kiitikadi.

Lakini watu hao waliachiliwa huru baada ya watu mashuhuri wa Marekani kuingilia kati wakiwemo marais wa zamani Bill Clinton na Jimmy Carter, ambao wote walikwenda Pyongyang.

Mwaka 2009, Bwana Clinton alishiriki mazungumzo ya kuwaachilia huru waandishi wa habari wawili wa Marekani, Laura Ling na Euna Lee, waliokua wakituhumiwa kuingia Korea Kaskazini kinyume cha sheria .

Walikamatwa baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la pili la nuklia, wote walihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela na kazi ngumu kabla ya kuachiliwa huru.

Wachunguzi wa mambo wanasema huenda Pyongyang inawatumia Wamarekani inaowashikilia kama kinga wakati kukiwa na hali tete katika eneo la rasi ya Korea.

Machi mwaka huu, Umoja wa Mataifa uliongeza vikwazo dhidi ya taifa hilo la kikomunisti kufuatia jaribio lake la nuklia Februari 12 na lile la kombora la masafa marefu Disemba mwaka jana.

Pyongyang ilichukizwa na hatua hiyo na mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini ilishuhudia Marekani ikionesha silaha za hali ya juu.

Pia ilitishia kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyopo eneo hilo na kusitisha mawasiliano muhimu na Korea Kusini.

Serikali hiyo ya kikomunisti iliwaondoa wafanyakazi wake kutoka ukanda wa kiviwanda wa pamoja kati ya Kaskazini na Kusini na kuwazuia wafanyakazi wa Korea Kusini kuvuka mpaka kuingia kwenye ukanda huo.

Serikali ya Korea Kusini imeahidi Dola za Kimarekani milioni 273, kama mikopo ya dharura kwa makampuni yaliyoathiriwa na kufungwa kwa ukanda huo wa Kaesong.