Rais wa Madagascar kutetea kiti chake

Image caption Rais Andry Rajoelina wa Madagascar

Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amesajili jina lake kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi wa Julai licha ya kusema kwamba hangegombea.

Jina lake limejitokeza katika orodha ya wagombea 41 wa Urais waliopitishwa na tume ya uchaguzi .

Bw Rajoelina, akiungwa mkono na jeshi ,alimgo'wa madarakani Marc Ravalomanana mnamo mwaka 2009,na kukitumbukiza kisiwa hicho katika machafuko ya kisiasa.

Baada ya chagizo kutoka nchi za kanda viongozi wote wawili walikubaliana kutogombea uchaguzi wa mwezi wa Julai.

Lakini mshauri maalum wa Bw Rajoelina amesema makubaliano hayo yalivunjwa pale mke wa Bw Ravalomanana , Lalao, kuamua kugombea.

"sasa mchuano uko wazi kwa kila mtu," Augustin Andriamananoro ameliambia shirika la habri la Reuters.

Mama Ravalomanana aliejea nchini mwezi Machi kutoka Afrika ya Kusini,ambako yeye na mume wake walikimbilia baada ya kungo'lewa madarakani.

Maafisa wa serikali nchini Madagascar wamezuia juhudi kadhaa za Bw Ravalomanana kurejea nchini,wakitaja kua na khofu za kuzuka machafuko.

Aliyekua Rais Didier Ratsiraka, mwenye umri wa miaka 76, ambae alikwenda uhamishoni kwa miaka kadhaa baada ya kushindwa na Bw Ravalomanana katika uchaguzi uliozusha ubishi mkali mnamo mwaka 2002, nae pia yumo katika orodha ya wagombea.

Bwana Rajoelina alipata umaarufu kama dj kabla ya kuingia katika siasa.

Mapinduzi ya 2009 yaliiacha Madagascar ikipigwa pande na jamii ya kimataifa na kunyimwa misaada na mataifa ya kigeni.