Waziri Kerry afika Moscow kuijadili Syria

Image caption Waziri John Kerry awasili Urusi kuijadili Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, yuko nchini Russia kujaribu kupunguza tofauti kati ya Washington na Moscow kuhusu mzozowa Syria.

Anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais Vladmir Putin mjini Moscow, lakini nchi hizo mbili hazikubaliani kuhusu mustakabal wa Rais Bashar al – Assad.

Russia ambayo inamuunga mkono rais Assad, imekataa kuunga mkono shinikizo la Marekani linalomtaka ajiuzulu. Hivi karibuni, Marekani ilidai kuwa haiwezi kuzungumzia lolote iwapo inawapatia silaha wapinzani wa Syria.

“kuwapatia silaha waasi, huo ni uamuzi,” alisema Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel wiki iliyopita.

Ziara ya Bw. Kerry inakuja siku chache baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga kusini mwa Syria.

Russia ililaani mashambulizi hayo, ambayo vyanzo vya Israel vinasema yalilenga makombora yaliyokuwa yakipelekwa kwa kundi la Hezbollah nchini Lebanon linalotishia utengamano wa ukanda wa Mashariki ya Kati.

Ikulu ya Moscow, Kremlin inasema Rais Putin tayari amezungumza na waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Kabla ya ziara ya Bw. Kerry, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitoa wito kwa nchi za magharibi kuacha ushabiki wa kisiasa kuhusu suala la silaha za kemikali nchini Syria, anaarifu mwandishi wa BBC mjini Moscow, Steven Rosenberg.

Ameongeza kuwa, hali hiyo inatia shaka na inatafsiri maoni kwamba dunia ilikuwa inaandaliwa kwa uwezekano wa kuishambulia kijeshi Syria.

Mchunguzi wa Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa umekanusha maoni yaliyotolewa na mmoja wa wataalam wake kwamba, kulikuwa na ushahidi wa waasi kutumia gesi ya sumu aina ya “Nerve”.

Mchunguzi wa umoja huo, Carla Del Ponte mapema alidai kuwa, ushahidi kutoka kwa waathirika na madaktari umeongeza shauku kubwa lakini pia si uthibitisho wenye utata kwamba wapiganaji waasi wametumia kemikali aina ya Sarin.

Lakini Tume ya Uchunguzi kuhusu Syria Jumatatu ilisisitiza kuwa haijafikia muafaka wowote kuhusu uchunguzi huo.

Gesi hiyo isiyokua na rangi wala harufu inaelezwa kuwa ni silaha ya maangamizi ya umma na imepigwa marufuku kutumika chini ya sheria za kimataifa.

Mjini Washington, msemaji wa ikulu ya Marekani, White House, Jay Carney, amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba, matumizi yoyote ya silaha za kemikali utakua umefanywa na vikosi vya serikali.

Marekani na Israel kwa pamoja zimeeleza kuwa matumizi ya silaha za kemikali katika mzozo wa Syria ni sawa na kubadilisha mwelekeo ambao unaweza kuchochea kuingilia kijeshi kwa jumuiya ya kimataifa.

Habari zinasema, haitakuwa rahisi kwa Bw. Kerry kubadilisha msimamo wa Rais Putin kuhusu Syria.

Ni jambo lililowazi kwamba, Moscow ina wasiwasi kuwa, hali mbaya ya sasa itazidi kuwa mbaya zaidi endapo Rais Bashar al – Assad atalazimishwa kuondoka madarakani na wanamgambo kushika hatamu za uongozi.

Baada ya ziara yake ya Russia, Bw. Kerry atakwenda Roma kukutana na maafisa wa Italia, Israeli na Jordan kujadiliana nao kuhusu masuala mbalimbali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo lile la mpango wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.