Bangladesh - Nusura baada ya siku 17

Image caption Mwanamke wa Bangladesh anusurika baada ya siku kumi na saba

Waokoaji nchini Bangladesh wamemuokoa mwanamke mmoja kutoka kwa vifusi vya jengo lililoporomoka yapata siku 17 zilizopita.

Zaidi ya watu 1000 wamethibitishwa kufariki wakati jengo hilo la orofa 8 lilipoporomoka nje kidogo ya mji mkuu Dhaka.

Miujiza

Waokoaji hao wametaja hilo kama miujiza. Ikiwa zimepita zaidi ya wiki mbili tangu jengo hilo la orofa nane kuporomoka, walikuwa tayari wameshaanza kukata tamaa ya kumpata mtu mwengine yoyote hai.

Lakini wanajeshi walipokuwa wanazoa zoa vifusi katika orofa ya chini walisikia sauti ikiita. Walitumia vifaa vyao maalum ambavyo vilionyesha dalili za uhai chini ya vifusi.

Mwanamke huyo aliitana akitaja jina lake kama Reshma. Baada ya juhudi za pamoja waokoaji pamoja na wanajeshi walifanikiwa kumtoa mwanamke huyo alikonaswa na kumkimbiza hospitalini.

Image caption waokoaji walianza kupoteza matumaini

Inaamioniwa kuwa aliweza kubakia hai kutokana na maji iliyokuwa imemiminwa humo ndani siku ya kwanza ya maporomoko hayo. Tukio hili pia limetajwa kama habari njema kwa kile kilichotajwa kama wiki mbili za majonzo na kupotea matumaini kwa taifa la Bangladesh.

Jamii ya kimataifa

Ajali hiyo ya Bangladesh imesababisha mataifa mengine hasa ya magharibi kama vile Uingereza kutilia shaka bidhaa za kutoka nchini Bangladesh kwa namna zinavyotengenezwa na uwezekano wa kunyanyaswa wafanyikazi.