Hayati Patrice Lumumba atunukiwa mji

Image caption Lumumba alichaguliwa kama waziri mkuu wa DRC mwaka 1960

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatarejiwa kujenga mji ambao utakuwa kumbukumbu na kwa mpiganiaji uhuru wa nchi hiyo Patrice Lumumba . Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali Lambert Mende.

Lumumba aliongeza kuwa, mji huo utakaojulikana kama Lumumbaville utazileta pamoja jamii mbili zilizoko katika eneo hilo.

Lumumba aliyekuwa mshirika wa nchi za muungano wa Kisovieti, alichaguliwa kama waziri mkuu mwaka 1960, baada ya zaidi ya karne moja ya utawala wa kikoloni.

Mauaji yake, yalitokea miezi minne baadaye alipokuwa na umri wa miaka 35 na Marekani na Uingereza ndizo zililaumiwa kwa kifo chake.

Mwezi Aprili, mmoja wa wabunge wa bunge la malodi nchini Uingereza alisema kuwa afisaa mmoja wa MI6, alimwambia kuwa Uingereza ilihusika na kifo cha Lumumba.

Mwandishi wa BBC mjini Kishansa anasema kuwa habari hii bila shaka itapokelewa vyema na wananchi wa DRC kwani Lumumba anasalia kuwa mtu mashuhuri.

Mji wa Lumumbaville utajengwa katika mkoa wa Kassai-Oriental ambako alizaliwa hayati Lumumba.

Ujenzi wa mji huo unatarajiwa kuanza mwaka 2014, aliongeza kusema bwana Mende.

Serikali inatumai kuwa wahisani watasaidia katika ujenzi wa mji huo na kuwa utakuwa kivutio kwa watalii.

Mwanawe Lumumba, Raymond, aliambia BBC kuwa babake angefurahia sana uamuzi wa serikali kujenga mji huo.

"alitaka Congo kuwa kitovu cha maendeleo barani Afrika," alisema Raymond Lumumba.

"kwa hivyo, angetaka uwe mji wa kisasa.''

DR Congo ina utajiri wa madini ingawa watu wengi wanaishi katika umaskini.

Nchi hiyo imekumbwa sana na mizozo kadha wa kadha tangu ijipatie uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Mzozo wa hivi sasa ambao umesababishwa na kundi la M23, ulianza mwaka jana Mashariki mwa nchi na kusababisha takriban watu 800,000 kutoroka makwao.