Watu wawili korokoroni kuhusiana na vifo vya watoto

Image caption Ramani ya Nigeria

Raia wawili wa Nigeria, wamehukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani, kuhusiana na mauaji ya takriban watoto Themanini ambao walipewa dawa za kuota meno yaliyokuwa na sumu.

Mahakama moja mjini Lagos waliwapata na hatia maafisa wa kampuni iliyotengeneza dawa hiyo iitwayo My Pikin.

Baada ya vifo vya watoto hao kuripotiwa uchunguzi ulifanyika mwaka wa 2008 na kubainika kuwa dawa hiyo ilikuwa na chemikali inayotumiwa kupunguza viwango vya joto, katika injini ya gari.

Jaji wa mahakama hiyo pia aliagiza kampuni hiyo kufungwa na mali yake yote kutwaliwa na serikali.

Dawa hiyo ambayo ilidaiwa kupunguza joto mwilini, ilitumika kutibu uvimbe katika fizi, iligunduliwa kuwa na chemikali ya diethylene glycol, inayotumika kwenye magari.

Uchunguzi wa madaktari ulibainisha kuwa sumu hiyo ilisababisha vifo miongoni mwa watoto hao baada ya figo zao kushindwa kufanya kazi.

Katika lugha ya Kipidgin inayotumika sana mjini Lagos Nigeria, My Pikin inamaanisha mtoto wangu