Mazishi ya Chinua Achebe yaanza

Mazishi ya mwandishi maarufu wa riwaya wa Nigeria, Chinua Achebe, yameanza katika mji wa Ogidi, kusini-mashariki mwa nchi ambako ndiko alikotoka.

Maziko yanaendelea kwa juma zima, kumkumbuka na kusherehekea maisha ya mmoja kati ya waandishi maarufu kabisa wa Afrika.

Bwana Achebe alifariki mwezi March akiwa na umri wa miaka 82.

Kongamano la waandishi, mihadhara ya wasomi na kanivali ni baadhi ya matukio katika mazishi ya wiki moja ya mwandishi Chinua Achebe.

Shughuli zitakuwa nyingi katika mji wa Ogidi alikozaliwa kusini-mashariki mwa Nigeria.

Wageni kutoka pembe zote za dunia wanatarajiwa kutoa heshima zao za mwisho kwa yule waliyemwita baba wa fasihi ya kisasa ya Afrika.

Bwana Achebe aliwakosoa viongozi wa Nigeria, hata hivo wanasiasa wengi maarufu wanatarajiwa kuhudhuria matanga yake.

Maziko yatafuata taratibu za Kikristo na utamaduni wa kabila lake la Igbo.

Chinua Achebe alikuwa maarufu kwa mtindo wake wa uandishi ambao umefuata mila ya kutoa hadithi ya kabila lake la Igbo.

Kitabu cha Chinua Achebe Things Fall Apart kimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 50.