Hali ya Sintofahamu yazuka Kismaayo

Image caption Kismaayo

Wajumbe kutoka Mataifa ya Muungano wa ustawi wa Mashariki na Upembe wa Afrika, Igad, waliwasili mwishoni mwa wiki katika mji wa Kismaayo, Kusini mwa Somalia, kudadisi uhalisi wa mambo kufuatia kuteuliwa kwa Marais wawili katika vikao wiwili tofauti.

Kufuatia hatua hiyo iliyotekelezwa juma lililopita wakaazi wa eneo hilo wamejawa na hofu kuwa huenda kukazuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe iwapo sintofahamu hiyo haitasuluhishwa kuweka utawala wa mji huo chini ya uongozi thabiti unaotambuliwa na kukubaliwa na pande zote zinazong'ang'ania mji huo.

Wajumbe hao walikutana na wazee wa Kisomali wa mji wa Kismaayo, na pia makundi yote yanaozozania kuthibiti mji huo. Wanapaswa kuwasilisha ripoti yao kwa mkutano wa marais wa Igad utatakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu, pembeni mwa mkutano wa Muungano wa Afrika kule Addis Ababa.

Kabla ya wajumbe hao kuwasili, watu kadhaa walitangaza kuwa walichaguliwa kuongoza eneo la Juba, mji mkuu yake ukiwa Kismaayo.

Sheikh Ahmed Madobe, ambaye aliongoza vikosi vya Somalia ambavyo vilisaidia wanajeshi wa Kenya wanaofanya chini ya Amisom kuuteka mji huo, alichaguliwa kama Rais waa eneo hilo.

Wakati huohuo Aden Bare Hiirale, ambaye ni kiongozi mashuhuri kule, alisema kuwa alichaguliwa na watu wa eneo hilo kama Rais wa Jubbaland. Serikali ya Somalia ilikataa uchaguzi huo, na kutoa wito kwa wanajeshi wa AMISOM walioko kule Kismaayo kutoegemea upande wowote.