Wakimbizi wa Syria mzigo kwa Jordan na Lebanon

Image caption Wakimbizi wengi wa Syria wametoroka na kuingia nchi jirani za Uturuki, Jordan na Lebanon

Shirika la misaada la Uingereza Oxfam, linasema Jordan na Lebanon zinahitaji msaada wa dharura kuwasaidia maelfu ya wakimbizi kutoka Syria waliokimbia mapigano nchini mwao.Oxfam linasema kuongezeka kwa joto na ukosefu wa maji na vyoo vya kutosha kunaongeza hatari za kiafya kwa wakimbizi hao.

Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi linasema zaidi ya raia milioni moja na nusu kutoka Syria wamesajiliwa rasmi kama wakimbizi.Kwa mujibu wa Oxfam, ni wazi kwamba wengi wa wakimbizi hao hawarudi nyumbani hivi karibuni na wenyeji wao yaani nchi za Lebanon na Jordan zinahitaji usaidizi wa dharura wa kimataifa.

Linasema wengi wa wanaovuka mpaka kutoka Syria huishia katika hifadhi zisizowasaidia kama vile maduka yasiokuwa na watu na maeneo mengine nje ya makaburi. Ukosefu wa maji na vyoo na kuongezeka kwa joto kunaongeza uwezekano wa kuzusha matatizo makubwa ya afya.

Oxfam linasema wafadhili wanapaswa kuzinduka na kukabiliana na ukweli wa mambo kwamba fedha zaidi zinahitajika.