Wapiganaji wa Boko Haram wakamatwa Maiduguri

Image caption Jeshi linasema wapiganaji kadhaa wametoroka na kuingia katikla nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon

Takriban wapiganaji 120 wamekamatwa katika mji wa Maiduguri, eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wakati walipokuwa wanaandaa mazishi ya kamanda wao. Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi.

Jeshi pia limeteka maeneo matano kutoka kwa wapiganaji hao.

Hata hivyo hakuna taarifa zengine kuthibitisha madai ya wanajeshi hao.

Rais Goodluck Jonathan, alitangaza sheria ya hali ya hatari katika majimbo matatu, Mashariki mwa Nigeria ili kutuliza hali ambayo imekuwa ikivurugwa na wapiganaji wa Boko Haram.

Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi na mauaji ya kupangwa tangu mwaka 2009, wakisema wanataka kuunda jimbo la kiisilamu nchini humo.

Kundi lengine la kiisilamu liitwalo Ansaru, lilijiunga na harakati za Boko Haram mwaka 2012 na limekuwa likiwateka nyara watalii.

Maafisa wanasema kuwa takriban watu, 2,000 wametoroka makwao na kuingia nchi jirani ya Niger, wakati wengine wakivuka na kuingia Cameroon,tangu jeshi kuanza operesheni yake dhidi ya wapiganaji hao katika majimbo ya Borno, Adamawa na Yobe wiki jana.

Wanajeshi 2,000, walipelekwa katike eneo hilo wiki jana katika operesheni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya wapiganaji hao wa kiisilamu.

Jeshi limesema kuwa pia linatuma wanajeshi wengine 1,000 Adamawa .

Wapiganaji wanaotoroka na kuingia nchi jirani za Chad na Niger wanadhibitiwa kulingana na Chris Olukolade.

"wanajeshi pia walisema waliona makaburi yanayoaminika kuwa ya wapiganaji waliozikwa kwa haraka huku wengine wakiwa njiai wakitoroka operesheni ya jeshi dhidi yao.''

Brigedia Gen Olukolade, alisema takriban wapiganaji 120 waliokamatwa wanahojiwa na kufikisha 200 idadi ya wale waliokamatwa na jeshi tangu wiki jana.

Wanamgambo walikamatwa huku wakijiandaa kwa mazishi ya kamanda wao aliyeuawa kwenye opereshi hiyo.

Jeshi hilo limeweza kuteka miji mitano na viji kutoka kwa wanamgambo hao katika maeneo ya mashinani katika jimbo la Borno, na kuaharibu kambi zote za wapiganaji hao.

Wiki jana Jeshi lilisema kuwa lilishambulia ngome za wapiganaji hao katika mbuga ya wanyama ya Sambisa Kusini mwa Maiduguri.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, ametaka jeshi la Nigeria kujizuia na kutokiuka haki za binadamu huku likiwasaka wapiganaji hao.