Afya ya Rais Bouteflika yazua wasiwasi

Image caption Baadhi ya vyombo vya habari vinasema Bouteflika yuko hali mahututi

Waziri mkuu wa Algeria amekanusha madai kuwa Rais Abdelaziz Bouteflika anaumwa sana akisema kuwa hali yake inaimarika kila siku mjini Paris.

Bwana Bouteflika, mwenye umri wa miaka 76, hajaonekana hadharani tangu kushikwa na kiharusi mwezi Aprili.

Waziri mkuu, Abdelmalek Sellal,amesema kuwa Madaktari wa Bouteflika wamemtaka apumzike kabisa wakati akiendelea kupata nafuu

Hali ya kiafya ya Bouteflika ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1999 imezua wasiwasi kuhusu uthabiti wa nchi Algeria.

Licha ya umri wake na afya yake inayozorota, kunao ambao bado wanaamini kuwa anaweza kuwania muhula wa nne katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao.

Wendesha wakuu wa mashtaka, wametaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya magazeti mawili yaliyoripoti kuwa Bouteflika yuko katika hali mahututi

Jarida la kifaransa la Le Point liliripoti kuwa bwana Bouteflika, aliyetibiwa Saratani mnamo mwaka 2005,yuko katika hali mbaya ya kiafya huku baadhi ya viungo vyake mwilini vikiwa vimeharibiwa.

Bwana Sellal, alisema kuwa habari za kupotosha zilizopeperushwa na baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu afya ya rais zinahujumu usalama na maendeleo ya vyombo vya habari vya Algeria.