Wengi wafariki kufuatia Kimbunga, Oklahoma

Image caption Watoto 20 wa shule ya msingi wanasemekana kufariki baada ya kimbunga kupiga shule yao

Kimbunga kikubwa kimepiga Jimbo la Oklahoma, nchini Marekani na kuharibu kabisa mitaa.

Maafisa wanasema zaidi ya watu tisini wamefariki, wakiwemo takriban wanafunzi ishirini ambao shule yao ya msingi iliporomoka.

Wanafunzi wengine wanahofiwa kufunikwa na vifusi.

Kimbunga hicho kilipiga mji wa Moore kwa takriban dakika arobaine, na kurusha magari katika vifusi vya nyumba na maduka.

Rais Obama ametangaza hali ya mkasa mkubwa na kuahidi usaidizi wa serikali kwa utawala wa jimbo hilo.

Takriban watu 120 wanaendelea kupokea matibabu hospitalini

Masaa kadhaa baada ya Kimbunga hicho kupiga, shughuli za kuwatafuta manusura ingali inaendelea.

Wanatumia mashine kubwa kujaribu kuwatafuta waliokwama chini ya kifusi ili kuwaokoa.

Mji wa Moore ulipigwa na kimbunga kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa muda wa miaka 14 wakati kimbunga kingine kikubwa kilipopiga eneo hilo.

Watu wengine zaidi wanajulikana kuuawa katika Kimbunga hicho.

Hospitali zimekuwa zikiwapokea majeruhi , wengine wakiwa katika hali mbaya zaidi na maafisa wa utawala wanaonya kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.

Maafisa wakuu wa serikali ya jimbo walitakiwa kuungana katika juhudi za kuwasaka manusura usiku kucha.

Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa afya, angalau watoto 20 walikuwa miongoni mwa wale waliofariki.

Shule ya msingi ya Plaza Towers ndiyo iliyoathirika zaidi kuliko sehemu zingine , kimbunga kiliharibu paa ya shule na kuangusha kuta zake zote.

Shule nyingine moja pia ilipigwa na kimbunga hicho lakini walimu walifanikiwa kuwaokoa wanafunzi.