Mlipuko wa Bomu waua watu 2 Goma DRC

Image caption Waasi wa M23 waliondoka Goma kufuatia shinikizo wa kidiplomasia mapema mwaka huu

Watu wasiopungua wawili wameuwawa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya, kufuatia mlipuko wa bomu mjini Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Ripoti zinasema watu wasiojulikana walirusha bomu hilo katika eneo moja lililokuwa na umati mkubwa wa watu.

Shambulio hilo limetokeo huku Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa huko Goma Ban Ki Moon akianza ziara yake katika eneo hilo.

Kwa siku ya tatu mfululizo majeshi ya serikali na waasi wa M23 wameshambuliana kwa roketti na risasi nje ya mji wa Goma ambao Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kuzuru hapo kesho.

Bwana Ban yuko nchini humo katika mwanzo wa ziara ya kuunga mkono juhudi za kutafuta amani katika eneo la Maziwa Makuu.

Ziara hiyo inaambatana na kuzuka upya kwa mapigano hayo ambayo yametia kikomo makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yametiwa saini kati ya serikali na waasi miezi sita iliyopita.

Umoja wa mataifa unajiandaa kutuma kikosi kipya cha kulinda amani ambacho kitakabidhiwa jukumu la kusalimisha silaha kutoka kwa waasi.

Wanajeshi wa serikali wamekabiliana na waasi wa M23 katika mapigano mazito karibu na mji wa Goma, Mashariki ya DRC tangu Jumatatu huku watu 19 wakiuawa.

Makabiliano ni ya kwanza tangu M23, kuondoka mjini humo mwaka jana kufuatia shinikizo za kidiplomasia.

Umoja wa mataifa unasema kuwa unaongeza kasi ya juhudi zake za kutafuta amani kwa kutuma kikosi cha wanajeshi 3,000 kujaribu kuzima mapigano ya hivi punde Mashariki mwa DRC

'Makombora na roketi'

Takriban watu 800,000 wametoroka makwao tangu waasi wa M23 kuanza uasi wao mwezi Mei mwaka jana.

Kombora lilianguka katika eneo la Ndosho linalopakana na Goma na kumuua mtu mmoja huku wanne wakijeruhiwa.

Duru zinasema kuwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili alifariki huku jamaa zake wakijeruhiwa vibaya.

Mwandishi wa BBC mjini Goma, Gabriel Gatehouse, anasema kuwa waasi na wanajeshi wa serikali wameshambuliana katika eneo la Mutaho, umbali wa kimomita 10 mashariki mwa mji wa Goma kwa siku ya tatu leo.

Wanajeshi wanne wa serikali pamoja na waasi 15 waliuawa kwenye makabiliano hayo Jumatatu, kulingana na msemaji wa serikali Lambert Mende.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kuzuru Goma siku ya Alhamisi akiambatana na rais wa benki ya dunia Yong Kim, kama sehemu ya kuhamasisha kuhusu amani na maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu.