Kerry asihi jeshi la Nigeria

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, ametoa wito kwa wakuu wa Nigeria kuhakikisha kuwa jeshi halivunji haki za kibinaadamu katika operesheni yake ya sasa dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu, kaskazini mwa nchi.

Bwana Kerry, ambaye anahudhuria sherehe za AU mjini Addis Ababa, alisema Marekani inaunga mkono kabisa juhudi za serikali ya Nigeria kufyeka mashambulio ya Boko Haram yaliyoendelea kwa miaka mine; lakini alisisitiza kuwa ukatili wa upande mmoja siyo kisingizio cha mwengine kufuata.

Marekani na makundi ya kutetea haki za kibinaadamu yamesema yametiwa wasi-wasi na tuhuma zinazoendelea kwamba wanajeshi wa Nigeria wamekiuka haki za kibinaadamu wakati wa kupambana na wapiganaji.

Ijumaa jeshi lilisema liliangamiza makambi kadha ya Boko Haram yaliyokuwa na zana za kutosha.

Awali mwezi huu Nigeria ilitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu ya kaskazini-mashariki.