Kenya kumbe yamjua Adebolaje

Wakuu wa Kenya na Uingereza wamethibitisha kuwa raia mmoja wa Uingereza - mmoja kati ya vijana wawili waliokamatwa kwa kumchinja mwanajeshi mjini London - alikamatwa Kenya zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje ya Uingereza imesema ubalozi wake Kenya ulimpa msaada wa kibalozi Michael Adebolajo.

Mkuu wa idara ya kupambana na ugaidi nchini Kenya, Boniface Mwaniki, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Bwana Adebolajo alikamatwa Novemba mwaka wa 2010, akishukiwa kujitayarisha kupigana pamoja na wapiganaji wa Kiislamu wa Somalia.

Msemaji wa serikali ya Kenya, Muthui Kariuki, anasema Bwana Adebolaje alipofungwa alikuwa na jina jengine, na ndio sababu hapo awali alikana kuwa mtu huyo aliwahi kwenda Kenya.

Aliiambia BBC kwamba baadae Adebolaje alikabidhiwa kwa wakuu wa Uingereza.

Hivi sasa watu 6 wanazuwiliwa na polisi wa Uingereza kwa kuhusika na mauaji ya mwanajeshi siku ya Jumatano.