Niger yaonya Libya yaweza geuka Somalia

Rais Mahamadou Issoufou wa Niger amesema kuwa fujo katika eneo hilo zinatoka Libya, na ameonya kuwa Libya inaweza kuwa kama Somalia.

Rais Issoufou alisema wapiganaji wa Kiislamu waliofanya mashambulio nchini Niger siku ya Alkhamisi walitoka kusini mwa Libya.

Inajulikana kuwa watu 35 waliuwawa katika mashambulio hayo dhidi ya kambi ya jeshi na mgodi wa uranium unaoendeshwa na Wafaransa.

Wapiganaji 10 ni kati ya watu waliouwawa.

Makundi ya wapiganaji wa Kiislamu walioteka sehemu kubwa ya Mali mwaka jana yamesema kuwa yamehusika na shambulio la Niger.

Waandishi wa habari wanasema tangu serikali ya Muammar Gaddaf kuondolewa miaka miwili iliyopita, pamekuwa na ukosefu wa sheria katika sehemu kubwa ya eneo la kusini mwa Libya.