Wafungwa kwa kushambulia ubalozi Tunisia

Image caption Maandamano nchini Tunisia

Mahakama nchini Tunisia imewapa watu 20 kifungo cha nje cha miaka miwili kila mmoja kwa kuhusika na shambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Tunis, Septemba mwaka 2012, mawakili wa watu hao wamesema.

Watu wanne walifariki katika vurugu wakati ubalozi wa Marekani na shule moja jirani, ziliposhambuliwa.

Waandamanaji wa kiisilamu walilenga kushambulia ubalozi huo wakati yalipofanyika maandamano kupinga kutengezwa kwa filamu ya kiisilamu iliyomkejeli Mtume Mohammad nchini Marekani.

Katika miezi ya hivi karibuni serikali imekuwa na msimamo mkali dhidi ya watu wenye itikadi kali.

Mapema mwezi huu mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji aliuawa wakati polisi walipokabiliana na wafuasi wa vuguvugu la Ansar al-Sharia mapema mwezi huu, viungani mwa mji mkuu Tunis.

Wakili wa washtakiwa, Anwar Oued Ali, aliambia shirika la habari la AFP, kuwa watashauriana na familia zao ikiwa wanataka kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama. Ikiwa wanataka tutafanya hivyo.

Hakuna tangazo rasmi kuhusu hukumu hiyo.

Pia jumanne mwanamume mmoja alifariki katika makabiliano kati ya polisi na wachuuzi, mjini Bizerte kuhusu sheria za uchuuzi.

Waziri wa mambo ya ndani alisema kuwa wachuuzi waliwarushia mawe polisi na mabomu ya petroli, ambapo polisi nao walijibu kwa kuwarushia gesi ya kutoa machozi.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa mwanamume huyo alifariki kutokana na moshi.

Mapinduzi ya kiraia yaliyomng'oa mamlakani rais Zine El Abidine Ben Ali mwezi Januri, mwaka 2011 yalichochea wananchi wa nchi jirani kuandamana na kupinga serikali zao