Kiongozi wa Al Shabaab Puntland akamatwa

Image caption Wanamgambo wa Al Shabaab

Maafisa wa utawala katika jimbo la Puntland, wanasema kuwa wamemkamata kiongozi wa kundi la al Shabab katika eneo hilo.

Maafisa wa usalama walimuonyesha hadharani kiongozi huyo anayejulikana kama Abdikafi Mohamed Ali baada ya kufanya msako nyumbani kwake mjini Bosaso siku ya Jumanne.

Wameelezea kuwa alijeruhiwa katika tukio la ufyatulianaji risasi ambapo mwanajeshi mmoja aliuawa.

Habari hii bila shaka ni pigo lengine kubwa kwa kundi la Wapiganaji wa Al shabaab hasa baada ya harakati za kijeshi kuendelea dhidi yao nchini Somalia.

Wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu tangu jeshi la Mungano wa Afrika kwa usaidizi wa wanajeshi wa Kenya kufanya harakati za kijeshi dhidi yao.

Wangi waliutoroka mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kutoka katika mji wa bandarini wa Kismayo ambayo ilikuwa moja ya ngome zao kuu.

Siku hizi kundi hilo limezindua mbinu nyingine ya kufanya mashambulizi hadharani kama hatua yao kulipiza kisasi.

Wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia mjini Mogadishu na viunga vyake kama ishara ya kuonyesha kuwa licha ya kufurushwa Mogadishu wangali wana uwezo wa kuendeleza mashambulizi. P[ia wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mpakani nchini Kenya kama hatua yao kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya kujihusisha na vita dhidi yao nchini Somalia.

Wadadisi wanasema kuwa Al Shabaab wanaonekana kushindwa nguvu ingawa kwa sababu ya upana wa mtandao wao na wao bado wana uwezo wa kulipiza kisasi.