Watoto Finland hulazwa kwa visanduku vya Karatasi?

Kwa miaka 75, kina mama wajawazito wamekuwa wakipewa na serikali visanduku vya karatasi. Visanduku hivyo vimekuwa vikitolewa kama sehemu ya vitu muhimu vya mwanzo kwa mtoto atakapozaliwa, kama vile vile nguo, mashuka na midori, ambavyo pia vinaweza kutumika kama kitanda. Na baadhi ya watu wanasema vitu hivyo vimeisaidia Finland kufanikiwa kuwa moja ya nchi ambayo ina viwango vya chini kabisa vya vifo vya watoto duniani.

Imekuwa ni desturi iliyojengekea ambapo visanduku vya karatasi hutolewa kwa mama wajawazito tangu miaka ya 1930 na imepangwa na serikali kutolewa kwa watoto wote nchini Finland, bila kujali hali ya familia wanazotoka, ni mwanzo wenye usawa katika maisha ya watoto.

Vifaa vya uzazi - ni zawadi kutoka serikalini na ipo kwa mama wote wajawazito.

Vifaa hivyo ni pamoja na nguo za mtoto, mfuko wa kulalia, vifaa vya kumbebea nje ya nyumba, sabuni za kuogea na mafuta ya mtoto, pamoja na nepi, matandiko na godoro dogo.

Godoro likiwa ndani ya kisanduku cha karatasi linakuwa kitanda cha kwanza cha mtoto. Watoto wengi kutoka familia zenye hali tofauti za maisha, kwanza wanalala katika sanduku salama la karatasi la pembe nne.

Mpango wa mwaka 1947 wa vifaa kwa mama mzazi, unampa chaguo la kuchukua sanduku hilo au kuchukua ruzuku ya fedha taslimu, ambayo kwa sasa ni euro 140, lakini asilimia 95% wanapendelea kuchukua sanduku ambalo lina thamani zaidi.

Utamaduni huuu umedumu tangu mwaka 1938. Kwa kuanzia, mpango huu uliwahusu tu familia zenye vipato vya chini, lakini ukabadilika mwaka 1949.

"Si tu kwamba uliwalenga wanawake wanaotarajia kujifungua lakini sheria mpya ilimaanisha, ili kupata ruzuku hiyo, au sanduku la mzazi, walitakiwa kumwona daktari au muuguzi wa zahanati ya manispaa kabla ya kufikisha miezi minne ya ujauzito," anasema Heidi Liesivesi, ambaye anafanya kazi Kela - Taasisi ya Bima ya Jamii ya Finland.

Kwa hiyo sanduku hilo linakuwa na vitu muhimu ambavyo mama wazazi wanatakiwa kuwa navyo kwa ajili ya watoto wao wachanga, lakini pia inasaidia wanawake wajawazito kuwa katika uangalizi wa madaktari na wauguzi wa serikali ya Finland.

Katika miaka ya 1930 Finland ilikuwa nchi maskini na kiwango cha vifo vya watoto kilikuwa cha juu ambapo katika kila watoto 1,000 waliozaliwa, 65 walifariki dunia. Lakini hali hiyo ilibadilika haraka katika miongo iliyofuata.

Mika Gissler, profesa katika Taasisi ya Taifa ya Afya na Ustawi mjini Helsinki, anatoa sababu kadha kuhusu hili- sanduku la uzazi na huduma za kabla ya uzazi kwa wanawake katika miaka ya 1940, ikifuatiwa na mfumo wa Bima ya Afya ya Taifa katika miaka ya 1960 na mtandao wa hospitali kuu.