Mkutano wa G8 wang'oa nanga Ireland

Image caption Hali ya usalama imedhibitiwa ambako kunafanyika mkutano wa G8

Viongozi wa dunia wanakutana Ireland Kaskazini kwa mkutano wa mataifa manane yenye uchumi mkubwa duniani G8.

Ajenda kuu ya mkutano huo itakua vita vya Syria. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema mkutano huo wa siku mbili utasaidia kutafuta mbinu ya kumaliza vita vinavyoendelea.

Marekani na Urusi zinaunga mkono mazungumzo ya amani. Hata hivyo pande mbili zinaunga mirengo tofauti. Marekani na washirika wake wa Ulaya, wanaunga mkono waasi huku Urusi ikiunga mkono utawala wa Syria.

Licha ya tofauti zilizopo kati ya msimamo wa Urusi na MarekaNi pamoja na washirika wao wa Ulaya, Bwana Cameron amesisitiza kuwa bado kuna baadhi ya mambo wanayokubaliana.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa pande zote zinaona umuhimu wa kuwepo mwafaka wa pamoja ili mzozo kukomeshwa na hicho ndicho anasema ni jukumu la mkutano wa G8.