Kesi dhidi ya Rais Kenyatta yaakhirishwa

Image caption Rais Uhuru Kenyatta

Mahama ya kimataifa ya ICC imeakhirisha siku ya kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta hadi tarehe 12 mwezi Novemba mwaka huu.

Hii ni kufuatia ombi la mawakili wa Rais Kenyatta kutaka kesi yao kuahirishwa hadi mwezi Januari mwaka ujao.

Mahakama iliamua kuwa upande wa Kenyatta unahitaji muda wa ziada ili kujiandaa ipasavyo kwa kesi, kwa sababu viongozi wa mashtaka walichelewa kufichua ushahidi walio nao dhidi ya rais Kenyatta.

Kenyatta anakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadmau wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya miaka sita iliyopita, akisemekana kuunga mkono mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya watu wa kabila moja.

Naibu Rais wa Kenya William Ruto naye pia anakabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kupanga mashambulizi dhidi ya jamii hasimu.

Majaji waliwaalika mawakili wa Uhuru Kenyatta kutoa maoni yao kuhusu muda wanaotaka ili kujiandaa kwa kesi dhidi ya mteja wao.

Baada ya kupokea maoni kutoka kwa upande wa utetezi, upande wa mashtaka, pamoja na waakilishi wa kisheria, majaji waliamua kuakhirisha kesi hiyo kutoka tarehe 9 Julai mwaka huu hadi Novemba.

Tarahe hiyo mpya ilifikiwa baada ya kuzingatia maswala mbali mbali ikiwemo haja ya upande wa mashtaka kujiandaa vyema kwa utetezi wao na mipango ya usafiri.

Rais Kenyatta ameshtakiwa kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya , makosa ya jinai ikiwemo, mauaji, kuwahamisha watu kinyume na sheria, ubakaji , mateso na vitendi vingine vya kinyama vinavyodaiwa kufanywa wakati wa ghasia hizo mwaka 2007/2008