Hali inatokota nchini Brazil

Image caption Raia wanpinga gharama ya kuandaa kwa kombe la dunia

Maandamano ya kupinga kupanda kwa nauli ya mabasi ,ufisadi na gharama ya kuandaa michuano ya kombe la dunia nchini Brazil sasa yameenea hadi takriban miji mia moja nchini humo.

Katika maeneo mengi, maandamano hayo yametibuka na kuwa ghasia ukiwemo mji wa Rio De Jeneiro ambapo waandamanaji waliwarushia mawe polisi, huku maafisa hao nao wakijibu kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi.

Waandamanaji hao pia wameyavamia majengo ya bunge na wizara ya masuala ya kigeni katika mji mkuu wa Brassilia.

Zaidi ya watu milioni moja wameshiriki maandamano hayo katika hatua ya hivi karibuni kuhusiana na mandamano ya kulalamika kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.

Ghasia zilizuka katika maeneo mengi na kusababisha kifo cha kijana mmoja mwenye umri wa miaka 18 mjini Sao Paulo.

Maandamano yalianza zaidi ya wiki moja iliyopita kulalamikia kupandishwa kwa nauli ya usafiri pamoja na kukithiri kwa rushwa huku wakilalamika pia kuhusu gharama ya maandalizi ya kombe la dunia mwaka ujao.

Rais Dilma Rousseff alisitisha safari yake nchini Japan ili kushughulikia mzozo huo.

Ameitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri utakaofanyika leo ili kujadili mzozo huo.

Yote haya yanakuja wakati Brazil inajiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia mwaka ujao.