Watu kumi wauawa Kismayo

Image caption Mwanajeshi wa Amisom mjini Mogadishu

Wakaazi wa mji wa Kusini wa Somalia Kismayo wanaendela kukikmbia makwao, kutokana na mapigano makali kati ya mababe wa kivita katika eneo hilo.

Takriban raia kumi wameuawa katika mapigano hayo yaliyotokea siku ya Ijumaa.

Mji wa Kismayo ni mji muhimu wa kiuchumi Kusini mwa Somalia na vita hivyo vimechochewa na ushindani mkali wa kithibiti biashara katika mji huo wa bandari.

Ripoti zinasema wapiganaji wa kundi la Ras Kamboni wanaoongozwa na mbabe wa zamani wa kivita aliyejitangaza kuwa rais wa eneo hilo Ahmed Madobe walikabiliana vikali na wapiganaji wa waziri wa zamani wa ulinzi wa Somalia Bare Hirale, ambaye pia anaongoza kundi lingine la waasi katika eneo hilo.

Hali ya Utulivu imeanza kurejea tena mjini humo ambao ni ngome ya zamani ya kundi la kigaidi la Kiislamu la Al Shabaab ambalo lina uhusiano na kundi la Al-Qaeda.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo mara moja, na kutoa wito kwa mababe hao wa kivita kusitisha uhasama kati yao ili kuepusha maafa zaidi ya raia wasiokuwa na hatia.

Wanajeshi wa Kenyan wanaohudumu nchini humo chini ya muungano wa Afrika wanamuunga mkono Bwana Madodbe, lakini serikali ya Somalia halimtambui kama rais na pia haijakubali uamuzi wake wa kutangaza kuwa eneo hilo limejitenga na Somalia.