Wanafunzi wakamatwa walevi Kenya

Image caption Wazazi waliofika kuwatafuta watoto wao waliokuwa wametoweka

Polisi wa Kenya wamewakamata zaidi ya wanafunzi elfu moja baada ya kupatikana wakiwa walevi mjini Nairobi wikendi hii.

Polisi waliendesha msako katika mabaa na vilabu vya burudani baada ya kupokea malalamishi kwamba watoto wa shule wamekua wakifurika kuburudika.

Kwa sasa wanafunzi wengi hawako shuleni baada ya waalimu wa Kenya kugoma wakitaka serikali kuwalipa marupurupu yao kutokana na ahadi iliyotolewa kwao na serikali mapema miaka ya themanini.

Mgomo huo umeingia wiki ya tatu sasa hali iliyofanya wanafunzi kukosa cha kufanya na hivyo kuanza kwenda kwenye vilabu vya burudani nyakati za usiku.

Katika kuzima tabia hii polisi mjini Nairobi mwishoni mwa wiki walifanya msako mkali katika mabaa na sehemu za burudani na kuwanasa watoto zaidi ya 1,000.

Polisi walianza kuwa na wasiwasI wakati visa vya unyang'anyi vilipoongezeka katika mji mikubwa nchini Kenya.

Wasiwasi ulizidi wakati walalamikaji walipokuwa wakidai kuwa wanaowapora na kuwapiga kabari ni kundi la watoto wanaodhaniwa kuwa ni wa shule.

Na mabaa na maeneo ya burudani ilipoanza kufurika polisi wakaona ni wakati muafaka wa kuchukua hatua.

Polisi sasa wametoa onyo kwa wenye mabaa nchini kenya kuheshimu sheria za biashara.

Baada ya wanafunzi kukosa kurudi nyumbani na wengine kuripotiwa kutoroka katika shule zao za mabweni wazazi walifurika katika vituo mbali mbali vya polisi kujua hatma ya watoto wao.

Lakini wengi wa wazazi waliokuwa wamefurika katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi walielekeza lawama zao kwa mgomo wa sasa wa walimu unaoendelea.

Polisi wanasema mtindo huu mpya wa watoto kutoroka madarasani na kuvamia maeneo ya burudani na ma baa sio tatizo la Nairobi pekee bali limeenea katika miji mingi ya Kenya.

Na kabla mambo hayaja haribika zaidi wazazi wanamtaka rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuingilia kati mgomu huo wa walimu kuhusu mishahara na marupurupu mbali mbali