Nelson Mandela angali hali mahututi

Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela angali hali mahututi ingawa madaktari wanaidhibiti hali yake. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya rais wa nchi hiyo Jacob Zuma.

Mandela aliyekuwa rais wa kwanza mwafrika wa Afrika Kusini ana umri wa miaka 94, alilazwa hospitalini tarehe 8 mwezi Juni akiwa anaugua maradhi ya mapafu.

Taarifa ya Zuma iliwashukuru wote waliomtumia ujumbe wa ugua pole Mandela nchini Afrika Kusini na kutoka kote duniani.

Wiki jana Rais Zuma alikanusha madai kuwa Mandela hana fahamu tena..

Watu waliomuona wanasema kuwa anaweza kusikia na hata kuhisi.

"tunashukuru umma wote kwa wale waliomuombea ili apate nafuu nje ya hospitali,'' ilinukuu taarifa ya Zuma ambayo ni ya kwanza katika siku tano zilizopita kuhusu hali ya Mandela.

Bwana Mandela anasifiwa kote duniani kwa ushujaa wake alipokuwa anapigania uhuru wa taifa hilo kutoka kwa wakoloni wazungu.

Alifungwa jela kwa miaka 27 kabla ya kuachiliwa huru mwaka 1990 na kuchaguliwa kama rais mwaka1994.

Hata hivyo alichaia madaraka baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miaka mitano.