Amri kumkamata kiongozi wa Brotherhood

Wafuasi wa Mohammed  Morsi

Mwendesha mashtaka mkuu wa Misri, ameagiza kukamatwa kwa kiongozi mkuu wa kundi la Muslim Brotherhood Mohammed Badie.Kiongozi huyo amelaumiwa kwa kuchochea ghasia zilizotokea mjini Cairo ambapo watu 51 waliuawa.

Amri ya kuwakamata viongozi wengine wapatao 100 wa kundi la Brotherhood imetolewa. Baadhi wamewekwa kizuizini. Agizo la sasa linajiri wakati Waziri Mkuu mteule yuko mbioni kuteua serikali mpya baada ya kuondolewa madarakani kwa Mohammed Morsi.

Kundi la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi limelaani muingilio wa jeshi la kutaja kitendo hicho kama mapinduzi. Wafuasi wake wamekua wakiandamana kila siku nje ya msikiti wa Rabaa Al-Adawiya wakitaka Morsi arejeshwe madarakani.

Chama cha kisiasa cha vuguvugu hilo, Freedom and Justice Party kimesema hakitajiunga na utawala wa mpito na kimekataa wadhifa wa uwaziri kilichotengewa na Waziri MKuu Hazem al-Beblawi.

Msemaji wa Muslim Brotherhood Gehad El- Haddad ameambia vyombo vya habari kwamba amri ya kumkamata Badie ni njama za jeshi kuzima maandamano. Kundi hilo limelaumu jeshi kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji wakati wakifanya maombi nje ya kambi kuu ya jeshi.

Kwa upande wake, jeshi limesema lilikua likijibu shambulio kutoka kwa waandamanaji waliokuwa na silaha. Makabiliano ya Jumatatu yalipelekea kuawa kwa zaidi ya wafuasi 50 wa Muslim Brotherhood.Kaimu Rais wa Misri, Adly Mansour ametangaza ratiba inayotoa muelekeo wa uchaguzi mpya nchi hio.

Hii ni pamoja na kufanyia marekebisho katiba iliyosimamishwa na jeshi na uchaguzi mkuu kufanyika mapema mwakani. Kwanza itaanza kura ya maoni dhidi ya rasimu ya katiba, uchaguzi wa bunge na baadaye uchaguzi wa Rais mpya mapema mwaka 2014.

Muungano wa upinzani wa National Salvation Front (NSF) ambao ulioongoza maandamano yaliyomuondoa madarakani Mohammed Morsi umepinga mpango wa sasa na kusema haukushauriwa. Muslim Brotherhood imepinga mpango wowote wa kuweka utawala mpya kando ya Bw Morsi.