Rais Al Bashir aondoka Nigeria ghafla

Image caption Bashir akipokelewa nchini Nigeria

Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameondoka Nigeria kufuatia wito wa kimataifa kukamatwa kwake kuhusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki dhidi yake katika jimbo la Darfur.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, liliwasilisha kesi mahakamani nchini Nigeria kujaribu kuishinikiza serikali ya nchi hiyo kumkamata rais Bashir ili kumkabidhi kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Bwana Bashir alikuwa Nigeria kwa mkutano ulioandaliwa na muungano wa Afrika kuhusu afya unaokamailika baadaye leo.

Ubalozi wa Sudan umesema kuwa aliondoka kwa sababu ya majukumu mengine.

Mahakama ya kimataifa ya ICC ilitoa kibali cha kumkamata Bashir mwaka 2009, baada ya kumtuhumu kwa kufanya mauaji ya halaiki wakati wa vita vilivyodumu mwongo mmoja katika jimbo la Darfur.

Sudan haitambui mahakama ya ICC na inaituhumu kwa kuwa chombo cha nchi za kimataifa kutumiwa kukandamiza nchi za Afrika huku Muungano wa Ulaya ukitoa wito kwa nchi za Afrika kutomkamata Bashir.

Aidha Bashir alitarajiwa kutoa hotuba kwenye mkutano huo mjini Abuja, Jumatatu kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

Lakini alipoitwa kutoa hotuba yake hakuwepo kwenye ukumbi.

Bashir alipokelewa na gwaride la jeshi Nigeria, alipowasili mjini Abuja Jumamosi. Mkutano huo unatafuta mbinu za kupambana zaidi na magonjwa ya Kifua kikuu, Ukimwi na Malaria.

Viongozi kutoka nchi nane za Afrika wanahudhuria mkutano huo.

Msemaji wa rais wa Nigeria,Reuben Abati, aliambia shirika la habari la AP kuwa Bashir alikuwa mjini Abuja kwa mwaliko wa muungano wa AU wala sio Nigeria.