Afueni kwa wafanyakazi wa nyumbani

Image caption wanawake wafanyakazi Saudi Arabia

Saudi Arabia imetangaza sheria mpya zinazotarajiwa kuwapa haki zaidi mamilioni ya wafanyikazi wa nyumbani.

Miongoni mwa sheria hizo ni kuwa waajiri watoe haki kamili kwa wafanyikazi zao.

Kwa upande wa wafanyakazi hao watahitajika kuwaheshimu waajiri wao na kuheshimu dini ya Kiislamu.

Kumekuwepo malalamiko mengi ya unyanyasaji unaofanyiwa wafanyikazi hao katika mikono ya waajiri.

Masaibu ya wanawake wanaofanya kazi kama wasaidizi wa nyumbani nchini Saudi Arabia yamezua hamaki nyingi miongoni mwa wanaharakati wa haki za binadamu kwa miaka mingi.

Katika tukio baya zaidi, baadhi yao hupigwa na waajiri wao, au kudhalilishwa ki ngono na hata kisaikolojia. Lakini wengi pia wanateseka kazini kwa maisha magumu bila kuheshimiwa na waajiri wao.

Sheria mpya zilizotangazwa na waziri wa kazi nchini humo zinatarajiwa kusuluhisha hili.

Sheria zenyewe zinaamrisha waajiri kuwalipa wafanyakazi wao mishahara yao kamili kwa muda walioagizana.

Waajiri pia wataskahiki kuwapa wafanyikazi wao siku moja ya mapumziko katika wiki, na kutowafanyisha kazi zaidi ya saa tisa kwa siku.

Sheria kwa waajiri

  • Walipe mishahara kamili kwa wakati unaofaa
  • watoe siku moja ya mapumziko kwa wiki kwa wafanyikazi wao
  • wasiwafanyishe kazi zaidi ya saa tisa kwa siku

Sheria hizo pia zinasema kuwa wafanyikazi wanafaa kuwaheshimu waajiri wao na wasiache kazi bila sababu nzuri. Hata hivyo changamoto kubwa ni kwa namna sheria hizi zitakavyotekelezwa.

Adhabu ya faini kali imewekwa kwa yeyote atakayevunja sheria hizi.

Mamilioni ya wafanyikazi wa nyumbani hutafuta ajira nchini Saudi Arabia wengi wao kutoka Ufilipino, Malaysia, Indonesia na hata mataifa ya Afrika.

Baadhi ya mataifa yamesitisha vibali kwa raia wao kusafiri nchini Saudi Arabia kufanya kazi za nyumbani kutokana na visa vilivyokithiri vya unyanyasaji.

Sheria kwa Wafanyakazi

  • Lazima waheshimu waajiri wao
  • Lazima waheshimu dini ya kiislamu
  • Wasiache kazi au kukataa maagizo bila sababu mwafaka.