Hotuba ya kwanza ya rais Adly Misri

Chama cha Muslim Brotherhood nchini Misri kimetoa wito kwa mamilioni ya watu kushiriki maandamano mengine dhidi ya hatua ya jeshi la nchi hiyo kumpindua kiongozi aliyechaguliwa Mohamed Morsi.

Katika taarifa yake, kiongozi wa Muslim Brotherhood Mohamed Badie, ametoa wito kwa jeshi kufikiria upya hatua yake na likubali wanachotaka watu.

Lakini katika hotuba yake ya kwanza tangu kuwa kaimu rais, Adly Mansour, ameahidi kuimarisha usalama na utulivu dhidi ya wale wanaotaka kuzusha ghasia nchini Misri

Wiki mbili baada ya jeshi kumwondoa mamlakani Mohammed Morsi, bwana Mansour alisema kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuna usalama na uthabiti.

Wakati huohuo, chama cha Muslim Brotherhood kimekataa kujiunga na baraza la muda la mawaziri lililotangazwa wiki hii.

"tunapitia kipindi kigumu, na baadhi wanataka vurugu ilihali tunataka kusonga mbele,'' alisema kaimu kiongozi wakati akitoa hotuba kwenye televisheni.

"tutapigana vita vya kuhakikisha kuna usalama na tutalinda mapinduzi.''

Bwana Morsi aliondolewa mamlakani tarehe tatu mwezi Julai katika kile wafuasi wake walisema ni mapinduzi ya kijeshi.

Jeshi hata hivyo linasema kuwa lilikuwa linatimiza mahitaji ya watu baada ya mapinduzi ya kijeshi.